Sergei Eisenstein
Sergei Mikhailovich Eisenstein (Kirusi: Сергей Михайлович Эйзенштейн Sergey Mihaylovich Eyzenshteyn}}; 23 Januari 1898 – 11 Februari 1948) alikuwa mwongozaji na mtayarishaji wa filamu katika Umoja wa Kisovyeti. Alikuwa kati ya waongozaji filamu wa kwanza walioandika juu ya nadharia ya filamu na hivyo kuweka msingi kwa sanaa changa ya filamu. Mtindo alioanzisha na kuendeleza ilikuwa kukata vipande vya filamu na kuviunganisha baada ya kupiga picha.
Mtoto na kijana
[hariri | hariri chanzo]Eisenstein alizaliwa katika familia yenye asili ya Kiyahudi-Kijeraminai mjini Riga katika jimbo la Latvia ya Milki ya Urusi. Baba yake Mikhail Eisenstein alikuwa mjenzi mkuu wa Riga. Kijana Sergei alimaliza cheti cha elimu ya sekondari nyumbani kwake Riga akaendelea kusoma ujenzi na usanifu majengo katika mji mkuu wa Urusi Sankt Peterburg. Mwaka 1918 alijiunga na harakati ya mapinduzi ya Oktoba akajitolea kuyatetea kama mwanajeshi wa Jeshi Nyekundu. Alihudumia kama mchoraji katika kikosi cha kisiasa cha kutangaza shabaha za mapinduzi. Katika kipindi hiki alipata nafasi ya kusoma lugha ya Kijapani akajifunza alama 300 za mwandiko wa kanji; baadaye alisema ya kwamba mwandiko wa Kijapani ulimshawishi katika filamu zake.
Mwongozaji wa maigizo
[hariri | hariri chanzo]1920 akarudi katika maisha ya kiraia akapata kazi kwenye nyumba ya maonyesho ya maigizo mjini Moscow. Hapa alijifunza mengi chini ya mwongozaji wa maigizo Vsevolod Meyerhold. Pamoja na hayo alisoma pia sanaa ya filamu akatumia filamu fupi kama sehemu ya maigizo aliyoongoza.
Filamu za kwanza
[hariri | hariri chanzo]1923 alianza kujishughulisha na filamu hasa. Filamu yake kubwa ya kwanza ilikuwa °Manowari Potemkin° (Kirusi Броненосец «Потёмкин» bronyenosyets potyomkin) iliyosimulia habari za uasi wa wanamaji kwenye manowari wakati wa mapinduzi 1917 iliyoongoza harakati ya kumpindua Tsar wa Urusi. Hii ilikuwa filamu bila sauti kwa sababu teknolojia hii haikubuniwa bado.
Akaendelea kuongoza filamu nyingine zilizotangaza ujumbe wa mapinduzi ya kikomunuisti na historia ya Kirusi kama vile Oktoba: Siku 10 zilizotikisisha dunia, Alexander Nevsky na Ivan wa kutisha.
Safari ya Ulaya na Marekani
[hariri | hariri chanzo]Katika miaka 1928 - 1930 alifanya safari ya Ulaya magharibi alipofundisha utungaji wa filamu katika miji mingi. Mei 1930 aliendelea kutembelea Marekani lakini hakupatana na mitindo ya Hollywood.
Msanii chini ya Stalin
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kurudi Umoja wa Kisovyeti wanasiasa wengine walimtazama kwa wasiwasi kwa sababu ya muda mwingi aliyokuwa nje. Alipelekwa chuo cha sanaa alipofundisha. Mwaka 1938 alipewa nafasi tena ya kuongoza fuilamu kutokana na azimio la Stalin mwenyewe. Hii filamu juu ya mshujaa wa historia ya Urusi Alexander Nevsky ilikuwa filamu ya sauti ya kwanza aliyoongoza. Filamu hii ilitumia historia ya kutoa onyo dhidi ya tishio kutika kwa siasa ya Dola la Tatu (Ujerumani chini ya Hitler). Lakini wiki chache baada ya kumaliza filamu hii Stalin alifanya mapatano na Hitler na filamu iliondolewa kwenye sinema zote za Umoja wa Kisovyeti. Hapo Eisenstein alipaswa kusubiri hadi 1941 wakati Ujerumani ilishambulia Umoja wa Kisovyeti katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia hadi fiamu ya Nevsky ilirudi katika sinema na kujulikana pia kimataifa.
Ivan wa Kutisha
[hariri | hariri chanzo]Filamu iliyofuata juu ya Tsar Ivan wa Kutisha ilitumia pia historia ya kirusi kama kielelezo jinsi ya kupambana na maadui wa nje kama sehemu ya jitihada za kushinda Ujerumani. Mtunga muziki alikuwa Sergei Prokofiev. Stalin alipenda filamu hii ikapewa tuzo la kitaifa. Lakini sehemu ya pili na ya tatu zilizofuata zilikataliwa na idara ya usimamizi wa uatmaduni wa chama cha kikomunisti kwa sababu Tsar huyu wa kutisha alianza kufanana mno na dikteta Stalin mwenyewe. Sehemu kubwa ya picha za sehemu ya tatu ziliharibika.
Mwisho wa maisha
[hariri | hariri chanzo]Afya ya Eisenstein ilipungua kutokana na matata haya yote akapata pigo la moyo akafa alipokuwa na umri wa miaka 50. Akazikwa kwenye makaburi ya monasteri ya Novodevichy mjini Moscow.