Nenda kwa yaliyomo

Madhehebu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Madhhab)
Dini na madhehebu yake leo ulimwenguni

Madhehebu (kutoka Kiarabu مذهب madhhab) ni mafundisho, maadili na matendo ya ibada yaliyo ya msingi katika dini fulani.

Hutumiwa pia kutaja makundi ndani ya dini fulani ambayo yanatofautiana bila ya kuvunja umoja wa msingi.

Historia inashuhudia hata leo kwamba madhehebu mbalimbali ya dini ileile yanaweza kushindana hata kupigana vita.

Asili ya neno

[hariri | hariri chanzo]

Kiasili neno la Kiarabu madhhab limetaja makundi ndani ya mafundisho ya masharti ya Uislamu yaliyotofautiana juu ya vipengele fulani vya shari'a. Likaendelea kutumiwa kutaja pia makundi makubwa ndani ya Ukristo na baadaye katika dini nyingine.

Madhehebu katika Ubanyani

[hariri | hariri chanzo]

Katika Ubanyani, tofauti ya madhehebu inategemea mungu yupi anaheshimiwa zaidi kati ya miungu mingi inayosadikiwa na waumini wa dini hiyo. Ndivyo yanavyotajwa Shaivism, Shaktism, Vaishnavism, Smartism na Halumatha.

Madhehebu katika Uyahudi

[hariri | hariri chanzo]

Wakati alipoishi Yesu Kristo, dini ya Uyahudi ilikuwa na madhehebu yaliyoshindana sana, hasa Masadukayo, Mafarisayo na Waeseni.

Baada ya mwaka 70, Yerusalemu na hekalu lake vilipobomolewa, walibaki Mafarisayo tu, lakini leo Wayahudi wanatofautiana tena hasa kati ya walioshikilia imani sahihi kadiri ya mapokeo na wale wanaotaka kujilinganisha zaidi na hali ya ulimwengu wa kisasa.

Madhehebu katika Ukristo

[hariri | hariri chanzo]

Wafuasi wa dini ya Ukristo, kutokana na wingi wao katika urefu wa historia na upana wa jiografia, wamegawanyika katika madhehebu mengi, kuanzia Kanisa Katoliki, Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki hadi makundi elfu kadhaa ya Uprotestanti ambayo yalitokea hasa kuanzia karne XVI na yanazidi kuongezeka siku kwa siku.

Pengine madhehebu kadhaa yanayojitegemea yanaweza kutazamwa kama jamii moja kutokana na asili, historia na misimamo yake (k.mf. Ushirika wa Anglikana au riti za mashariki na magharibi za Kanisa Katoliki).

Baadhi ya Wakristo wanaona mafarakano hayo kuwa mabaya sana, wakizingatia ombi la Yesu kwamba wafuasi wake wawe na umoja ili ulimwengu upate kumuamini. Kwa sababu hiyo wanashughulikia ekumeni ili kurudisha umoja kamili kati yao bila kufuta tofauti zisizovuruga umoja wa msingi.

Madhehebu katika Uislamu

[hariri | hariri chanzo]

Uislamu hugawiwa katika mikondo miwili mikubwa ambayo ni Wasunni na Washia.

Washia ndani yao wamegawanyika katika makundi mengi zaidi.

Kati ya Wasunni kuna madhehebu au madhhab manne yanayokubaliwa rasmi. Hali halisi makundi mengine ya Kisunni kama Wahabiyya yanaweza kuitwa madhehebu pia. Madhehebu manne yanayokubaliwa kati ya Wasunni ni Washafi'i, Wahanbali, Wamaliki na Wahanafi yaliyopokea majina kutokana na walimu wakuu wa kihistoria Muhammad ibn ldris ash-Shafi'i, Ahmad ibn Hanbal, Malik ibn Anas na Abu Hanifa.

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.