Sayari
Sayari (kwa Kiingereza planet) ni kiolwa kikubwa cha angani kinachozunguka jua (au nyota nyingine) na kung'aa kutokana na nuru ya jua iliyoakisiwa, tofauti na nyota na jua zinazong'aa peke yake. Kwa macho inaonekana kama nyota, lakini baada ya kuitazama kwa muda wa mwaka inaonekana inabadilisha mahali pake angani, tofauti na nyota kwa jumla. Tofauti kubwa kati ya sayari na nyota ni kwamba, nyota ukiitazama inametameta ila sayari haiwezi.
Jina
Jina la Kiswahili "sayari" lina asili yake katika neno la Kiarabu كوكب سيار kaukab sayar "nyota inayosogea" [1]. Neno hilo la Kiarabu linalingana au ni tafsiri ya neno la Kigiriki πλανήτης planetes (lenye maana ya "yenye kusogea") ambalo ni asili ya jina "planet" kwa Kiingereza na lugha nyingine za Ulaya.
Tangu zamani watazamaji wa anga katika tamaduni mbalimbali walitambua ya kwamba nyota kwa kawaida hukaa mahali pamoja lakini nyota chache zinabadilisha polepole mahali pake kati ya nyota nyingine zikifuata njia zinazorudia kila mwaka. Nyota hizo ziliitwa "nyota zinazosogea".
Ufafanuzi wa sayari
Zamani kulikuwa na sayari 5 tu zilizoonekana angani kwa macho matupu kama nyota zinazobadilisha mahali[2]. Tangu kupatikana kwa mitambo kama darubini miaka 400 iliyopita idadi ya violwa angani vyenye miendo ya pekee imeongezeka sana lakini imeonekana pia kuna tofauti kubwa sana kati ya violwa hivi.
Hivyo wataalamu wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU) walikubaliana mwaka 2006 kuhusu ufafanuzi wa sayari. Kiolwa cha angani kinahesabiwa kuwa sayari kama kinatimiza masharti matatu:[3]
- (c) kama ni kiolwa tawala cha obiti yake na hivyo limeondoa violwa vingine kwenye obiti kwa graviti yake.
Ufafanuzi huo uliamuliwa kwa kura hata kama wanaastronomia wengine hawakukubali. Azimio hili liliondoa hadhi ya sayari kwa Pluto [4] iliyowahi kutazamwa kuwa sayari katika miaka iliyopita.
Wakati mwingine kuna violwa vingine ambavyo vinavyoitwa pia "sayari" ingawa havitoshelezi masharti yote matatu.
- Violwa vya angani katika mfumo wa jua letu yenye umbo la kufanana na tufe yasiyolingana na sharti c) huitwa "sayari kibete" - kwa mfano Pluto.
- Violwa vinavyozunguka nyota nyingine nje ya mfumo wa jua letu, kama yana masi ya kutosha, huitwa "sayari za nje" (ing. exoplanet). Hadi Mei 2016 kuna 2125 zilizotambuliwa [5].
- Violwa vyenye masi ya sayari ambazo si sehemu ya mfumo wa jua lolote lakini zinapita angani zinazoweza kuitwa sayari bila nyota (ing. wandering planets, starless planets, siku hizi zaitwa pia "planemo").
Majina ya sayari
Kwa Kiswahili kuna tofauti kuhusu majina ya sayari kati ya vikundi viwili:
- sayari zinazoonekana kwa macho matupu ambazo ni Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohali. Hizi zilijulikana tangu kale na mabaharia hasa walizitumia kwa kukadiria njia wakiwa baharini mbali na bara. Majina haya yamepokelewa na Waswahili wa Kale kutoka kwa lugha ya Kiarabu pamoja na majina mengi ya nyota.[6] Ila sayari ya pili yaani Zuhura ambayo ni sayari inayong'aa kuliko zote pia ina jina la Kibantu ambayo ni Ng'andu ("mwenye kung'aa). Kwa lugha za Ulaya kama Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani majina ya sayari za jua letu yanatokana na majina ya miungu ya Roma ya Kale au Ugiriki ya Kale.
- sayari zisizoonekana kwa macho kama Uranus na Neptun pamoja na sayari kibete (Pluto) zilitambuliwa tu bada ya kupatikana kwa mitambo ya darubini. Hatua hii ya kiteknolojia ilitokea Ulaya na hivyo wataalamu wa Ulaya waliendelea katika desturi ya kutumia majina yenye asili katika lugha za kale Kigiriki na Kilatini. Elimu ya sayari hizi za nje zilizokuwa geni kwa mataifa yote mengine ya dunia ilisambaa pamoja na majina ya Kiulaya na hivyo lugha nyingi zinatumia majina haya.
Sayari za jua letu
Jua letu lina sayari nane ambazo ni Utaridi (Mercury), Zuhura (pia: Ng'andu; Venus), Dunia yetu (Earth), Mirihi (Mars), Mshtarii (Jupiter), Zohali (Saturn), Uranusi na Neptuni.
Toka mwaka 1930 hadi Agosti 2006 Pluto ilikuwa ikitambulika kama sayari hivyo kufanya idadi ya sayari zinazojulikana kuwa tisa. Hata hivyo chama chenye mamlaka juu ya masuala ya sayari na nyota, Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kimetangaza rasmi kuwa Pluto si sayari na kuiita sayari kibete[7]. Vitabu vingi vya shule vimebadilishwa kulingana na uamuzi huo, japo bado kuna vitabu ambavyo bado vinaonyesha Pluto kuwa sayari kweli.
Sayari tano za Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohari [8] huonekana kwa macho kama nyota angani. Lakini tangu zamani zilitambuliwa kuwa tofauti kwa sababu hazikai mahali palepale kama nyota ya kawaida bali huhamahama angani. Kutokana na tabia hii zimetazamwa mara nyingi kuwa na nguvu za pekee au hata kuwa miungu. Unajimu umetumia mwendo wa sayari zinazoonekana kwa macho kama msingi muhimu wa makadirio yao.
Sayari nyingine katika mfumo wa jua zimetambuliwa tangu kutokea kwa astronomia ya kisayansi kwa darubini. Hizi ni Uranus na Neptun. Katika lugha ya Kiswahili sayari zinazoonekana kwa macho huwa na majina ya asili ya Kiarabu isipokuwa Zuhura ina jina la Kibantu la Ng'andu pamoja na jina la asili ya Kiarabu. Majina mengine ni ya asili ya Kilatini.
Jumla ya jua, sayari zote 8 pamoja na miezi yao, sayari kibete, vimondo, nyotamkia na asteroidi inaitwa mfumo wa jua.
Aina za sayari
Sayari za jua letu hutofautiana kwa ukubwa na muundo. Mshtarii (Jupiter) ni sayari kubwa na masi yake ni mara 318 masi ya dunia yetu. Sayari ndogo ni Utaridi na masi yake ni takriban nusu ya dunia.
Kutokana na umbali tunatofautisha "sayari za ndani" kuanzia Utaridi (Mercury) hadi ukanda wa asteroidi, halafu "sayari za nje" kuanzia Mshtarii (Jupiter) hadi Uranus.
Muundo wa sayari ni tofauti; kuna vikundi kulingana na mata inayojenga sayari:
- Sayari za mwamba: sayari hizi zina muundo unaofanana na dunia yetu; asilimia kubwa ya masi ni mwamba. Hizi ni sayari za ndani za mfumo wa jua letu. Zote ni ndogo kuliko sayari za nje.
- Sayari jitu za gesi: sayari hizi kama Mshtarii (Jupiter) na Zohali (Saturn) ni kubwa na zimefanywa na hidrojeni na heli. Masi ya Mshtarii ni mara 318 ile ya dunia, Zohali mara 95. Ilhali sayari hizi ni baridi kutokana na umbali mkubwa na jua, hidrojeni inapatikana kwa kiasi kikubwa katika hali mango na kwenye sehemu za ndani hidrojeni ina tabia kama metali kutokana na shinikizo kubwa.
- Sayari jitu za barafu: hizi ni Uranus na Neptun. Ni kubwa kuliko dunia, lakini si kama sayari jitu za gesi; Uranus huwa na masi 14 za dunia, Neptun na masi 17 za dunia. Ganda la nje ni mchanganyiko wa hidrojeni na methani, na sehemu za ndani ni barafu ya maji na methani.
Sayari nje ya mfumo wa jua letu
Wataalamu wa astronomia wamegundua sayari-nje (ing. exoplanets) yaani sayari zilizoko nje ya mfumo wa Jua letu zinazozunguka nyota mbalimbali. Kutokana na umbali mkubwa na matatizo ya utazamaji kwa muda mrefu hakukuwa na uhakika kama nyota kuwa na sayari ni jambo la kawaida angani au kama sayari ni chache tu.
Tangu 1995 kuwepo kwa sayari-nje kuliweza kukadiriwa kutokana na mabadiliko ya mwendo wa nyota kadhaa yaliyoweza kuelezwa tu kutokana na masi ya karibu inayobadilisha mwendo wa kawaida. Baada ya kuboreshwa kwa vifaa vipimo vya mabadiliko ya mng'aro vimeonyesha mipito ya sayari, maana wakati wa kupita kwa sayari kati ya nyota fulani na mtazamaji duniani sayari inafunika sehemu ya nyota yake, hivyo mng'aro wake unapungua. Kiasi cha mabadiliko ya mng'aro kinaruhusu kukadiria umbali wa sayari na nyota yake na ukubwa wake. Sayari-nje nyingi zimetambuliwa kwa kutumia mbinu huu. Kutokana na maendeleo ya darubini imewezekana tangu mwaka 2004 kutambua sayari-nje kadhaa moja kwa moja lakini idadi yao hadi sasa ni ndogo wa sababu ugunduzi ni vigumu.
Hadi Aprili 2019 kuwepo kwa sayari-nje 4,048 kumethibitishwa na kati ya hizi mifumo ya sayari 659 imetambuliwa ambako kuna zaidi ya sayari moja.[9]
Nyingi kati ya hizo zilikuwa na ukubwa kufanana na Mshtarii au kubwa zaidi. Lakini sayari ndogo zaidi zimetambuliwa pia. [10]
Marejeo
- ↑ kutoka chanzo سير sair "kutembea, kusafiri"
- ↑ Hizi ni Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohali. Pale mwanzoni, kabla ya uchunguzi wa Kopernikus, haikueleweka ya kwamba Dunia ni sayari sawa na hizo nyingine.
- ↑ Azimio 5A ya IAU ya 2006 "The IAU members gathered at the 2006 General Assembly agreed that a "planet" is defined as a celestial body that (a) is in orbit around the Sun, (b) has sufficient mass for its self-gravity to overcome rigid body forces so that it assumes a hydrostatic equilibrium (nearly round) shape, and (c) has cleared the neighbourhood around its orbit." Tangazo kwenye Tovuti ya IAU, IAU 2006 General Assembly: Result of the IAU Resolution votes, iliangaliwa Mei 2016
- ↑ Pia na violwa vingine kama vile Ceres, Pallas, Juno na Vesta. Hizi nne zilitazamwa kuwa sayari tangu kutambuliwa mnamo 1801 hadi kuitwa “asteroidi” kwenye miaka ya 1850. When did the asteroids become minor planets? Archived 21 Septemba 2007 at the Wayback Machine., Hilton, James L. kwenye tovuti ya U.S. Naval Observatory, iliangaliwa mwaka 2008
- ↑ Schneider, Jean (16 January 2013). "Interactive Extra-solar Planets Catalog". The Extrasolar Planets Encyclopaedia. ilitazamiwa 8 Mei 2016
- ↑ Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97
- ↑ BBC
- ↑ kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1].
Menginevyo kuhusu mchangayiko wa majina ya sayari angalia ukurasa wa majadiliano. - ↑ Kamusi ya sayari za nje kwenye intaneti, ilizatamiwa 01 Mei 2018
- ↑ Schneider, Jean (10 Septemba 2011). "Interactive Extra-solar Planets Catalog". The Extrasolar Planets Encyclopaedia. Iliwekwa mnamo 2018-05-01.
Viungo vya nje
- Tovuti ya International Astronomical Union
- http://www.bbc.com/news/science-environment-33462184
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sayari kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |