Nenda kwa yaliyomo

Misri

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Wamisri)
Jamhuri ya Kiarabu ya Misri (Kiswahili)
Gumhūriyyat Misr al-ʿarabiyya (Kiarabu)
Bendera ya Misri Nembo ya Misri
(Bendera ya Misri) (Nembo ya Misri)
Lugha rasmi Kiarabu
Mji Mkuu Cairo
Mji Mkubwa Cairo
Serikali Jamhuri
Rais Abdel Fattah el-Sisi
Eneo km² 1,010,408
Idadi ya wakazi 100,075,480 (2020)
Wakazi kwa km² 99
Uchumi nominal Bilioni $302.256
Uchumi kwa kipimo cha umma $3,047
Pesa Lira au Pauni ya Misri = 100 Piaster
Kaulimbiu "Haki - Amani - Kazi"
Wimbo wa Taifa 'Biladi, Biladi, Biladi (nchi yangu, nchi yangu, nchi yangu)
Misri katika Afrika
Saa za Eneo UTC +2
Mtandao .eg
Kodi ya Simu +20

Misri (kwa Kiarabu: مصر, Masr) ni nchi ya Afrika ya Kaskazini-Mashariki ikiwa na eneo la Rasi ya Sinai kwenye bara la Asia pia.

Ni nchi yenye wakazi milioni 100 na mji mkuu Kairo ni kati ya miji mikubwa zaidi duniani (zaidi ya milioni 9).

Ni kati ya nchi za dunia zenye historia ndefu inayojulikana.

Jina la nchi

  • Jina la Misri kwa Kiswahili linalingana na jina rasmi la مصر Miṣr katika lugha ya Kiarabu. Ni jina la Kale jinsi inavyoonekana katika Biblia ya Kiebrania ambako inaitwa Mitzrayim (מִצְרַיִם, wingi wa Misri kumaanisha Misri ya Juu na Misri ya Chini). Maana ya jina hili ni "nchi".
  • Majina ya Kizungu ya "Egypt" (ing.), "Egypte" (far.), "Ägypten" (jer.) yanatokana na jina la Kigiriki Αίγυπτος (aigyptos). Hakuna hakika juu ya maana asilia ya neno. Wengine huamini neno limetokana na jina la hekalu muhimu mjini Memphis. Neno hili ni pia asili ya jina "Wakopti" na hii ni jinsi wenyeji wa Misri walivyojiita wakati wa utawala wa Dola la Roma

Jiografia

Misri imepakana na Bahari ya Mediteranea, Israel, Eneo la mamlaka ya Palestina, ghuba ya Suez, ghuba ya Aqaba, Bahari ya Shamu, Sudan na Libya. Umbo la nchi hufanana na trapeza.

Tabianchi ni yabisi sana na maeneo makubwa ni jangwa, pamoja na oasisi na maeneo ya savana ya miiba. Karibu wananchi wote huishi ndani ya kanda nyembamba ya bonde la mto Naili. Bonde hili linavuka nchi kuanzia mpakani na Sudani katika kusini kuelekea kaskazini hadi mdomo wa mto kwenye Bahari ya Mediteranea. Ardhi pande zote mbili za mto inamwagiliwa na kulimwa. Kwatika umbali mdogo kutoka mto jangwa inaanza.

Takriban kilomita 250 kabla ya mdomo Naili inagawanyika katika mikono mbalimbali na kuunda delta ya mto.

Kanda hili bichi si zaidi ya asilimia 5 za eneo lote la nchi, ila 98% za wananchi wote huishi humo. Kwa hiyo Naili huitwa "Baba wa Misri", kwa maana bila mto huo pasingekuwepo taifa hili.

Mji mkuu wa Kairo uko mwanzoni mwa eneo la delta.

Nchi yote huwa na kanda asilia zifuatazo:

  • Delta ya Naili: upande wa kaskazini wa Kairo Naili inajigawa katika mikono miwili mikuu na kati ya mikono hiyo miwili kuna eneo la delta yenye km² 23,000 kwa umbo la pembetatu. Inajaa ardhi ya rutuba kutokana na matope ya Naili iliyopelekwa huko na mafuriko katika muda wa miaka elfu kadhaa. Eneo hili linalimwa kote na kumwagiliwa likiwa na mikono midogo ya kando ya Naili.
  • Jangwa la Magharibi: ni eneo kubwa upande wa magharibi wa Naili lisilo na milima mikubwa. Kaskazini mwake kuna tambarare ya Lybia iliyo takriban mita 240 juu ya uwiano wa bahari. Kusini mwake linainama eneo la mbonyeo wa Qatara hadi mita 133 chini ya UB, halafu jangwa linapanda tena juu kuelekea kusini magharibi.
Ndani ya eneo hili kubwa kuna beseni kadhaa pamoja na oasisi za Siwa, Bahariyya, Farafra, Dakhla na Charga. Kilomita 100 upande wa kusini-magharibi wa Kairo kuna oasisi kubwa ya Fayyum pamoja na ziwa la Warun lenye eneo la km² 230.
  • Jangwa la Mashariki: ni eneo upande wa mashariki wa mto Naili. Huko kuna milima inayopanda juu ya mita 2,000 pamoja na wadi yaani bonde kali. Jangwa linatelemka hadi mfereji wa Bahari ya Shamu ambao ni sehemu ya Bonde la Ufa linaloanza Palestina na kuendelea hadi Ziwa Nyasa.
  • Rasi ya Sinai: ni eneo la jangwa na milima inayofikia hadi mita 2637 (Jabal Katharina).

Historia

Makala kuu: Historia ya Misri

Nchi hiyo ni kati ya vitovu vya ustaarabu wa binadamu, na kwa sababu hiyo inavutia watalii wengi.

Historia ya awali

Katika kipindi cha historia ya awali tangu takriban miaka 6000 KK wakazi wa Misri walikuwa na kilimo cha nafaka. Walikuwa na teknolojia ya Zama za Mawe. Wakati ule Jangwa la Sahara lilipanuka na kuwalazimisha watu kukaa karibu zaidi kwenye mto Nile na kwenye oasisi kama Faiyum.

Katika mazingira ya jangwa bonde la Nile liliwavuta watu kutokana na rutuba kubwa ya ardhi iliyoongezwa kila mwaka upya kwa njia ya mafuriko yaliyotandaza matope kutoka nyanda za juu kwenye ardhi.

Utafiti wa akiolojia umegundua ya kwamba wakazi hao wa bonde walianzisha tamaduni mbalimbali zilizokuwa tofauti kati yao lakini zilizowasiliana kibiashara. Mifano ya kwanza ya mwandiko wa hiroglifi imepatikana kwenye vyungu vilivyofinyangwa mnamo 3200 KK.

Misri ya Kale

Katika karne zilizofuata, mnamo 3000 KK yalitokea muungano wa sehemu mbalimbali wa Misri chini ya wafalme wenye nguvu wanaotajwa kwa cheo cha farao. Katika historia iliyotungwa na waandishi Wagiriki wa Kale ni kwa kawaida Farao Menes anayetajwa kuwa mtawala wa kwanza aliyeunganisha Misri ya Kaskazini na Misri ya Kusini kuwa milki moja. Lakini leo hii inajulikana kuna wafalme waliomtangulia waliokuwa tayari na milki kubwa. Hata hivyo Menes alianzisha utawala wa nasaba mbalimbali zilizofuatana, pamoja na vipindi vya kati ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe na mafarakano katika nasaba ziliweza kugawa nchi tena kwa muda.

Mafarao wa Misri ya Kale walifaulu mara kadhaa kupanua mamlaka yao hadi ndani ya Sudani ya leo, na pia kwa vipindi juu ya sehemu za Palestina na Syria ya leo. Mara kadhaa wavamizi kutoka nje walifaulu kushika utawala juu ya Misri kama vile Wahyksos kutoka Palestina / Kanaan, Wakushi kutoka Nubia au watu kutoka Lybia. Wavamizi hao walitumia pia cheo cha Farao wakijaribu kuendeleza tabia nyingi za milki za awali. Hatimaye wote walipinduliwa tena na viongozi wazalendo walioanzisha nasaba mpya.

Mwaka 525 KK mfalme wa Uajemi aliteka Misri. Kwa kipindi kifupi Wamisri waliweza kuwaondoa tena na kuendelea chini ya watawala wazalendo.

Misri ya Ptolemi (Wagiriki) na chini ya Roma

Uvamizi wa Aleksander Mkuu mwaka 332 KK ulianzisha kipindi cha Misri ya Kigiriki. Mji mpya wa Aleksandria ulikuwa mji mkuu mpya. Jemadari wa Wagiriki walitumia pia cheo cha Farao na kutawala kama nasaba ya Ptolemi, lakini tabaka ya watawala ilikuwa na utamaduni tofauti sana na wananchi wakulima wa kawaida.

Wakati wafalme Wagiriki waliendelea kutawala milki mpya ilienea kutoka magharibi ya Mediteranea iliyokuwa Dola la Roma. Malkia wa mwisho wa Misri alikuwa Kleopatra. Baada ya kifo chake Misri ilikuwa jimbo la Dola la Roma.

Utawala wa Kiroma uliendelea kwa karne 6. Katika muda huu Ukristo ulianza kuenea katika Misri. Nchi ilikuwa haraka kitovu muhimu cha imani mpya na Ukristo wa Kikopti uliendeleza liturgia na mapokeo ya pekee na kupeleka mfumo huu wa Ukristo hadi Sudani na Ethiopia.

Lakini hali ilikuwa ngumu baada ya magavana wa Roma na baadaye wa Bizanti kujaribu kuwalazimisha Wakopti kufuata liturgia na mafundisho ya Kanisa rasmi yaani Kanisa la Kiorthodoksi.

Uvamizi wa Kiarabu na Misri ya Kiislamu

Kwenye mwaka 639 jeshi la Waarabu Waislamu lilivamia Misri na kuteka nchi yote katika muda wa miaka 3. Wenyeji wengi waliokuwa Wakristo Wakopti hawakuwapinga kwa sababu walipendelea Waislamu kuliko Wakristo Waorthodoksi waliowahi kuwakandamiza vikali katika miaka iliyotangulia. Kwa karne kadhaa idadi kubwa bado walikuwa Wakristo lakini kuanzia karne ya 12 idadi ya Waislamu ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu Wakristo walipaswa kulipa kodi zaidi na vipindi kadhaa vya mateso vilitokea na yote ilisababisha kuhamia kwa wananchi kwenda dini mpya.

Watawala wapya hawakutumia Aleksandria kuwa mji mkuu bali walianzisha mji mpya wa Fustat karibu na Babylon ya Misri[1], pale ambako mto Nile unajigawa na kuanzisha delta yake.

Hadi mwaka 969 Misri ilitawaliwa na watawala Waislamu Wasunni waliokuwa kwa jina magavana na wawakilishi wa makhalifa huko Dameski au Baghdad, lakini zaidi watawala wa kujitegemea hali halisi. Mwaka 969 Wafatimi kutoka sehemu za Tunisia ya leo walivamia na kuteka nchi wakianzisha ukhalifa wao. Wafatimi walikuwa Waismaili, wakati ule mwelekeo wa kimapinduzi ya Shia. Walianzisha makao makuu yao nje ya Fustat na Babylon wakaiita "Al-Qahira", yaani mwenye ushindi, na hii ilikuwa chanzo cha Kairo ya leo.

Wakati wa vita za misalaba Wafatimi walishindwa na askari wa Wasunni waliendelea kuunda nasaba ya masultani wa Mamluki wa Misri.

Jimbo la Milki ya Osmani

Mnamo mwaka 1517 Waosmani walivamia na kuteka Misri. Hadi karne ya 19 Misri ikaendelea kama jimbo la Milki ya Osmani, kisheria hata hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Hali halisi nchi ilikuwa na kipindi kifupi kama milki ya kujitegemea wakati wa karne ya 19, hadi kusimamiwa na Uingereza hasa kwa shabaha ya kutawala mfereji wa Suez na kushuka kwa ngazi ya nchi lindwa.

Mwaka 1914 ilitangazwa kuwa nchi lindwa chini ya Uingereza; tangazo la uhuru la mwaka 1922 bado liliacha athira kubwa kwa Uingereza.

Uhuru

Tangu mwaka 1952 Misri imepata uhuru kamili, na tangu hapo ilitawala pia mfereji wa Suez.

Watu

Msongamano (watu kwa kilometa mraba).

Wakazi wengi (91%) ni Wamisri asili. Wengine ni Waazaba, Waturuki, Wagiriki, Wabeduini, Waberberi, Wanubi n.k. Wahamiaji kutoka Sudan na nchi nyingine ni milioni 5 hivi, wakati Wamisri wanaoishi ugenini ni milioni 2.7.

Lugha rasmi ni Kiarabu Sanifu cha Kisasa, wakati wananchi wanatumia kwa kawaida aina mbalimbali za Kiarabu, hasa Kiarabu cha Kimisri (68%)

Upande wa dini, sheria zinazitambua 3 tu: Uislamu, ambao ndio dini rasmi, Ukristo na Uyahudi.

Uwiano wa wafuasi wa dini hizo haujulikani vizuri, lakini Waislamu (hasa Wasunni) ni kama 90%, Wakristo (hasa Wakopti wanaoendelea kufuata Ukristo uliokuwa unatawala kabla ya Waarabu kuteka nchi katika karne ya 7) ni walau 10%, wakati Wayahudi wamehama karibu wote.

Tazama pia

Tanbihi

  1. Leo hii sehemu zote mbili ziko ndani ya Jiji la Kairo

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Serikali
Taarifa za jumla
Biashara
Mengineyo


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira
Makala hii kuhusu maeneo ya Misri bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Misri kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.