Nenda kwa yaliyomo

Grafolojia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Grafolojia (kutoka maneno ya Kigiriki γραφή, grafé, 'andiko' na λόγος, logos, 'elimu'[1]), ambayo pia huitwa elimu ya mwandiko, ni fani inayojaribu kutambua nafsi ya mtu kupitia jinsi anavyoandika.

Msingi wa elimu hiyo ni kwamba hatuandiki kwa mkono tu, kwa kuwa huo unaongozwa na ubongo. Mtu anapoacha kuiga herufi alizofundishwa kwa kuwa amezoea kuandika, anakuja kutokeza nafsi yake mwenyewe katika upekee wake. Tunaweza kusema mtu anapoandika bila kuzingatia usanifu wa herufi anajichora jinsi alivyo.

Wataalamu wa fani hiyo wanazingatia hasa kama mwandiko ni wa mviringomviringo au una pembe na ncha, unakandamiza karatasi kwa nguvu au la, ni mkubwa au mdogo, ni mpana au mwembamba, unapendeza kwa ulinganifu wa herufi zake au la, unafanyika kwa kasi au polepole, unakwenda wima ingawa karatasi haina mstari au huenda ukapanda ama kushuka, unaelekea upande gani, una mapambo au la, n.k.

Kila sifa ya mwandiko ina sababu yake na hivyo kudokeza silika ya mtu upande wa akili, utashi n.k. Lakini baada ya kuzizingatia zote ni muhimu kuziona kwa pamoja ili kumtambua mtu mzima jinsi alivyo, na hatimaye kumsaidia maishani.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Tangu zamani sana, watu kadhaa wa China, India, Ugiriki na Italia walivutiwa na jinsi mwandiko wa kila mmoja ulivyo tofauti na ule wa wengine, wakaona unadokeza nafsi yake.

Kuanzia karne XVII vilianza kutungwa vitabu kuhusu suala hilo, mpaka ikapatikana ile inayodaiwa na baadhi kuwa sayansi ya mwandiko (grafolojia) inayochunguza uhusiano kati ya mwandiko wa mtu na undani na nafsi yake (akili, maelekeo, vipawa, umbo, maradhi n.k.).

  1. "Fine Dictionary". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-09-24. Iliwekwa mnamo 2014-09-22.