Historia ya Iran
Historia ya Iran inahusu eneo ambalo leo linaunda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tangu mwaka 500 KK makabila madogo ya nchi hiyo yaliunganishwa, na hii ilikuwa mwanzo wa milki ya Uajemi. Mfalme Koreshi II aliunganisha Uajemi wote chini ya mamlaka yake akavamia sehemu za Uturuki wa leo na Babeli na kuunganisha nchi hizo.
Waandamizi wake walipanua milki hadi Misri, Uhindi na Ugiriki.
Milki hiyo ilikwisha baada ya kushindwa na Aleksanda Mkuu; lakini nasaba za Waparthia na Wasasanidi waliendelea kufufua milki ya Uajemi tena na tena.
Baada ya uvamizi wa Waarabu Ujaemi ukatawaliwa kwa muda kama sehemu ya ukhalifa wa Uislamu lakini baada ya karne kadhaa nasaba za kieneo zilichukua utawala kwa jina la khalifa ila hali halisi kama watawala wa kujitegemea.
Baada ya uvamizi wa Wamongolia nasaba ya wana wa Timur iliunganisha Uajemi pamoja na Afghanistan na Asia ya Kati.
Tangu mwaka 1600 kitovu cha utawala kilirudi Uajemi wenyewe chini ya nasaba za Safawi na Khadjari.
Baada ya vita vikuu vya kwanza vya dunia afisa wa kijeshi Reza Khan alimaliza utawala wa Wakhadjari akaanzisha nasaba ya Pahlavi. Alijaribu kuleta matengenezo ya kimaendeleo nchini akaiga katika mengi mfano wa Atatürk katika Uturuki jirani.
Utawala wa kifalme ulikwisha mwaka 1979 wakati wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Ayatollah Ruholla Khomeini yaliyoanzisha Jamhuri ya Kiislamu.
Kipindi kifupi baada ya mapinduzi Uajemi ilishambuliwa na Iraki na vita vya miaka 8 vilisababisha vifo vingi.
Uhusiano na nchi za magharibi, na hasa Marekani, umekuwa mgumu tangu mapinduzi hayo, hasa baada ya wanafunzi Waajemi kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Teheran na kuwateka Wamarekani. Fatwa ya Ayatollah Khomeini kudai kifo cha mwandishi Salman Rushdie iliongeza sifa za ukali za Uajemi.
Tangu uchaguzi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2006 aliyetamka matishio dhidi ya nchi ya Israeli kuna mashaka juu ya mipango ya Uajemi kupanua teknolojia yake ya kinyuklia kwa hofu ya kwamba serikali yake inalenga kujenga bomu la nyuklia. Mapatano yalichukua miaka hadi kufikiwa mwaka 2015.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Iran kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |