Nenda kwa yaliyomo

Sala

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Yesu akisali katika mateso yake huko Gethsemane kadiri ya Heinrich Hofmann.
Mwanamume Mshinto wa Japani akisali peke yake.
Wanawake Wakristo wa Urusi wakisali pamoja.

Sala (kutoka neno la Kiarabu صلاة‎, ṣalāh; pia maombi) ni njia ambayo binadamu anauelekea ulimwengu wa roho, hasa kwa nia ya kuongea na Mungu kwa sauti au kimoyomoyo.

Malengo yake yanaweza kuwa tofauti: kusifu, kushukuru, kuomba au kujiachilia.

Upande wa pili sala ni kutafakari ili kusikiliza na kuelewa ujumbe wa Mungu.

Sala inaweza kufanywa na mtu peke yake au na wengi pamoja, hata kwa kuimba.


Sala katika dini mbalimbali

Dini zinaelekeza waumini wake kusali kwa namna mbalimbali.

  • Uislamu unatofautisha sala, pia swala inayofuata utaratibu maalum na dua ambayo si namna huru ya kumwomba Mungu. Katika Uislamu sala inatakiwa mara 5 kwa siku. Dua ni sala za hiari. Zulia inatumika kwa ajili ya kumsujudia Mungu.

Katika Ukristo

Katika Kanisa Katoliki

Suala la nguvu ya sala kwa Mungu linawahusu watu wote, hata wenye dhambi ya mauti, kwa sababu hawawezi kustahili lakini wanaweza kusali. Ombaomba alichonacho ni ufukara wake tu, lakini ndicho kinacholitia nguvu ombi lake; mtu akiomba kwa moyo wote, huruma inamuinamia. “Kwa kweli na haki umeyaleta hayo yote juu yetu kwa sababu ya dhambi zetu… Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako” (Dan 3:29,34). Zaburi zimejaa maombi ya namna hiyo.

Waumini wanapaswa kujiuliza: je, tunaisadiki nguvu ya sala? Kishawishi kinapotaka kutuangusha, au tunapokosa mwanga, au msalaba unapobebeka kwa shida, je, tunakimbilia sala alivyotuambia Yesu? Haitutokei kuitilia shaka, kimatendo kama si kinadharia? Ingawa tunajua ahadi yake, pengine tunadhani tumesali tusisikilizwe. Tunaona nguvu ya mashine, ya jeshi na ya pesa, lakini hatusadiki vya kutosha nguvu ya sala, kwa sababu hatujui vizuri inatokea wapi na tunasahau inaelekea wapi.

Asili ya mito iko juu, katika maji ya mvua: huo ni mfano wa sala ambayo nguvu yake inatokea juu vilevile. Pengine tunashawishika kudhani sala asili yake ni sisi ambao kwa njia yake tunajaribu kuvuta matakwa ya Mungu upande wetu kwa kumbembeleza. Papo hapo dhana hiyo inagongana na hakika ya kwamba hakuna anayeweza kubadili matakwa ya Mungu wala kuyavuta upande huu au huu. Mungu ni wema unaotaka kujitoa tu, ni huruma iliyo tayari daima kusaidia, lakini pia ni yule asiyebadilika hata kidogo, wala utashi wake haubadiliki milele. “Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu” (Mal 3:6). Kwa maongozi yake, utaratibu wa viumbe na wa matukio umeshapangwa tangu milele: “Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu, ajute” (Hes 23:19). Mbingu na dunia “zitaharibika, bali wewe utadumu, naam hizi zitachakaa kama nguo; na kama mavazi utazibadilisha, nazo zitabadilika. Lakini wewe u yeye yule, na miaka yako haitakoma” (Zab 102:26-27). “Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka” (Yak 1:17). Kama ni hivyo basi, je, tukubali kuwa sala haiwezi kitu na hivyo hata tukisali vizuri yatatukia yanayotakiwa kutukia?

Neno la Injili linabaki palepale, na maisha ya Kiroho yanapaswa kupenywa nalo zaidi na zaidi. “Amin, amin nawaambia: Mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu” (Yoh 16:23). Ni kwamba sala haina asili ndani mwetu, wala si juhudi ya kumfanya Mungu abadili mipango yake. Kwa kweli matakwa yake hayabadiliki hata kidogo, lakini ndiyo asili ya hakika ya nguvu ya sala. Hilo ni jepesi kueleweka, ingawa ndani yake limo fumbo la neema. Kwanza tusisitize kuwa sala halisi inapata kwa hakika inachokiomba kwa sababu Mungu asiyeweza kukanusha aliyosema ameamua iwe hivyo.

Kujichorea picha ya Mungu asiyetaka wala kujua tangu milele sala zetu ni dhana ya kitoto sawa na ile ya kuamini Mungu anaweza kubadili mipango yake ajilinganishe na matakwa yetu. Tangu milele maongozi yake yamekwishapangwa yote: si yatakayotokea tu, bali pia namna ambayo yatokee, na sababu zitakazofanya yatokee. Kwa ajili ya mavuno Bwana ameandaa mbegu, mvua na jua. Vilevile upande wa roho ameandaa neema zinazohitajika kwa utakatifu na wokovu. Katika ngazi zote, kwa ajili ya matokeo fulani Mungu ameandaa sababu zitakazofanya yapatikane. Basi, sala ni sababu iliyokusudiwa naye ituletee zawadi zake, hasa Roho Mtakatifu: ndiye paji lenyewe ambalo tumeandaliwa na kupaswa kuliomba.

Uhai wa viumbe vyote ni zawadi ya Mungu, lakini mtu tu anaweza kujitambua hawezi kuishi kibinadamu wala Kimungu pasipo zawadi hiyo. Basi, si ajabu kwamba Mungu amempangia ajiombee zawadi. Hapa pia amekusudia kwanza tokeo la mwisho, halafu njia au sababu zitakazoliwezesha. Kisha kuamua atupatie, amepanga tusali ili kupokea, kama baba aliyepanga kuwafadhili wanae lakini ameona afadhali waombe fadhili hiyo. Zawadi ya Mungu ndiyo tokeo; sala ndiyo sababu itakayoliwezesha. “Watu wanapaswa kujiandaa kwa sala wapokee yale ambayo Mwenyezi Mungu amepanga kuwapatia tangu milele” (Gregori Mkuu). Hivyo ni lazima tuombe misaada tunayohitaji ili kutenda mema na kudumu mpaka mwisho, kama ilivyo lazima tupande mbegu ili kuvuna. Wapo wanaosema, eti! “Tusali tusisali, yatatukia yaliyopangwa”. Tuwajibu, “Huo ni upumbavu sawa na kusema tutavuna iwe tumepanda au la”. Maongozi ya Mungu ni tofauti na imani potofu hiyo kwa kuwa yanaheshimu hiari ya binadamu. Bila shaka tunahitaji neema ya msaada ili kusali, lakini hiyo inatolewa kwa wote, yaani wanaikosa wale tu wanaoikataa. Tofauti na mbegu, ambazo zinaweza zikashindwa kuzaa, sala halisi, dumifu, nyenyekevu na yenye tumaini ambayo mtu anajiombea misaada ya lazima kwa wokovu haipotei kamwe. “Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Lk 11:10-13).

Basi, tuamini sala: siyo nguvu ya kibinadamu yenye asili ndani mwetu, bali chemchemi ya nguvu yake imo ndani ya Mungu na ya stahili zisizo na mwisho za Mwokozi. Inashuka toka mpango wa milele wa upendo na kupanda juu hadi huruma ya Mungu. Hivyo tunainua utashi wetu hadi utashi wake ili tutake pamoja naye yale aliyopanga tangu milele atupatie. Sala, badala ya kutaka kumuinamisha Mungu kwetu, ni “kuinua roho kwa Mungu” (Yohane wa Damasko).

Kama ni hivyo, kinyume cha kupinda maongozi yake, sala inayachangia. Badala ya kutaka mmoja, tunataka wawili pamoja. Kwa mfano, maombi yetu mengi kwa uongofu wa mtu yakisikilizwa, tuseme, Mungu ndiye aliyemuongoa, lakini ametujalia tushiriki kazi yake hiyo, akipanga tangu milele tuombe hata neema hiyo itolewe. Namna hiyohiyo tunachangia wokovu wetu tukijiombea neema za lazima kuupata, ambazo baadhi yake (k.mf. kufa katika neema inayotia utakatifu) hazistahiliki ila zinapatikana kwa sala. Hivyo neema ya kukingiwa dhambi ya mauti haistahiliki (la sivyo tungestahili chanzo cha stahili, yaani kudumu katika neema inayotia utakatifu), lakini tunaweza kuipata kwa sala. Hata neema ya kuzamia sala, ingawa haistahiliki, inapatikana kwa kuomba. “Mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa” (Yak 1:5). Pia neema ya uongofu kwa mtu anayeonekana kuikataa, tunaweza kutumaini tutaipata kadiri tulivyo wengi na tunavyodumu kuiomba.

Mungu amepanga sala iwe njia ya kufikia utakatifu na wokovu, hivyo ina nafasi katika maisha ya roho, kama vile joto upande wa mwili. Basi, lengo la roho ni uzima wa milele, na mema yanayotufikisha huko ni ya aina mbili: yale ya Kiroho yanayohusika moja kwa moja, na yale ya kimwili yanayoweza yakachangia wokovu kadiri yanavyobaki chini ya yale ya Kiroho.

Mema ya Kiroho ni: neema inayotia utakatifu na zile za msaada, maadili, vipaji saba vya Roho Mtakatifu na stahili zinazotokana navyo. Sala inaweza yote ili kumpatia mkosefu neema ya uongofu, na mwadilifu neema ya kudumu katika wajibu wake. Sala hiyohiyo inaweza yote ili kutupatia imani hai zaidi, tumaini imara zaidi, upendo motomoto zaidi, uaminifu mkubwa zaidi kwa wito wetu. Tunavyoelekezwa na Baba Yetu tuombe kabla ya yote kwamba jina la Mungu litukuzwe kwa njia ya imani yenye kung’aa; kwamba ufalme wake ufike, inavyotarajiwa na tumaini, na kwamba atakalo lifanyike kwa upendo ulio safi na wa nguvu zaidi na zaidi. Sala inaweza pia kutupatia mkate wa kila siku kadiri unavyohitajika au unavyofaa kwa wokovu wetu, hasa mkate wa ekaristi pamoja na misimamo ya kufaa ili kuupokea vema. Inatupatia tena msamaha wa makosa yetu na kutuandaa tusamehe jirani; inatukinga na kishawishi au kutupa nguvu tukishinde. Lakini, ili sala iweze kupata hayo yote ni lazima itimize masharti tuliyoorodhesha: iwe nyofu, nyenyekevu (anayeomba ni maskini); ijae tumaini kwa wema usio na mipaka ambao hatutakiwi kuwa na shaka nao; idumu ili kutokeza hamu kubwa ya moyo. Ndivyo ilivyokuwa sala ya mama Mkananayo aliyeambiwa, “Na iwe kwako kama utakavyo” (Math 15:28).

Hata kama Bwana anatuacha tupambane na matatizo makubwa tuliyoomba atuepushe nayo, tusidhani hatusikilizi. Kwamba tu tunaendelea kusali, maana yake Aliye juu anatusaidia, kwa sababu pasipo neema mpya za msaada tusingeendelea kusali. Anatuacha tupambane na matatizo ili tujifunze kupiga vita, tutambue kuwa hivyo vinatuletea faida, kuwa neema tuliyojaliwa inatosha tuendelee kupambana ambako nguvu ya Bwana inayochochea ya kwetu inajitokeza wazi zaidi: “Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu” (2Kor 12:9). Ndivyo tunavyohakikisha katika kutakaswa hisi na roho, tunapopaswa kuomba mfululizo neema ya hakika ambayo peke yake inaweza kutukinga na udhaifu wowote.

Kuhusu mema ya kimwili, sala inaweza kutupatia yale yote yanayokusudiwa kutusaidia kwa namna moja au nyingine tuelekee uzima wa milele: chakula, afya, nguvu, mafanikio. Sala inaweza kuyapata, mradi tuombe kabla na juu ya yote kwamba tumpende Mungu zaidi na zaidi: “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa” (Math 6:33). Tusipopata mema hayo ya kimwili ni kwa sababu hayatufai kwa wokovu, lakini kama sala imefanyika vizuri tutapata neema nyingine muhimu zaidi. “Bwana yu karibu na wote wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu” (Zab 145:18). Sala ya kuomba ikiinua kweli roho kwa Mungu, itaandaa kufanya sala bora zaidi ya kuabudu, ya kufidia, ya kushukuru na hatimaye ya kuungana naye.

Kanisa Katoliki lina maombi bayana sana ambayo wote walioko kanisani husali kwa pamoja[1]. Maombi hayo hufunzwa kwa wote wanaoshiriki kanisani tangu wakiwa wachanga ili waweze kuiga wazee wao. Maombi hayo ni kama majibu ya Misa, rosari, maombi ya waumini, maombi ya toba na kujuta dhambi. Ni lazima Mkatoliki ajue vizuri sala hizo ili kuamini katika Ukristo na kushiriki kikamilifu ibada [2].

Katika Uislamu

Mikao muhimu ya salat katika baadhi ya madhehebu ya Uislamu.

Sala inayotakiwa kutolewa na kila Mwislamu mara tano kwa siku hufuata utaratibu ufuatao kadri ya utaratibu wa Uislamu wa Kisunn[3]i:

1. Kutia nia 2. Kusimama katika swala ya faradhi pamoja na kuweza 3. Takbiri ya kufungia Swala 4. Kusoma Fatiha 5. Kurukuu 6. Kuitadili kwa kulingana sawa baada ya kurukuu 7. Kusujudu kwa viungo saba 8. Kukaa baina ya sijida mbili 9. Kukaa kwa Atahiyatu ya mwisho. 10. Kusoma Atahiyatu 11. Kumswalia Mtume ﷺ katika Atahiyatu ya mwisho. 12. Kutoa salamu 13. Kujituliza katika nguzo zote 14. Kutungamanisha baina ya nguzo

Tazama pia

Tanbihi

  1. Taz. Misale ya Waamini, toleo la mwaka 2021, uk. 1495-1535
  2. "Prayer of the faithful Catholic wedding". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-09-24. Iliwekwa mnamo 2017-10-20.
  3. https://www.al-feqh.com/sw/namna-ya-kuswali Namna ya kuswali

Viungo vya nje

Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.